1000 Scholars Swahili Translation

Sisi kundi la wasomi waliotia sahihi nakala hii, twailekeza barua hii kwa utawala wa Kanisa la Orthodoksi na kwa wakristo wote wa kanisa hili kote ulimwenguni na kwa watu wenye heri njema. Tunaiandika barua hii kutokana na nia ya kuleta umoja au uwiano ambao kupitia kwake maisha mapya ya kristo yatadhihirika kwa  mwanadamu. Tunaomba kwamba mkutano huu wa baraza hili ambao ni wa kwanza kulishughulikia swala la umoja wa kanisa unaotarajiwa kuandaliwa na unaosubiriwa kwa hamu na ghamu utazaa matunda mema ya roho mtakatifu. Kwa mintarafu hii, sisi tunaidhinisha mkataba wa viongozi wa Orthodoksi uliotangazwa wazi katika mkutano wa Umoja wa Orthodoksi katika Sinodia uliofanyika Januari 2016. Mkutano huo ulikubaliana kuwe na kikao cha Baraza Takatifu na Kuu la Crete katikati mwa mwezi wa Juni 2016.

Tunaamini kwamba hakuna vizingiti vyoyote vile katika kuanzisha kikao hicho mwezi wa sita licha ya maswali mengi yaliyoulizwa kuambatana na rasimu za utafutaji umoja na taratibu za kufuatwa kuafikia lengo hilo. Tunathibitisha kuwa baadhi ya maswala yaliyoulizwa ni ya haki kwa mfano kufunguliwa kwa rasimu za awali zilizokusudiwa kuleta umoja kwa Kanisa la Orthodoksi. Tunahisi kwamba kuna vilevile maswala mengine ibuka ya Kanisa hili ya karne ya ishirini na moja yanayohitaji kuangaziwa katika vikao vijavyo vya kuleta uwiano wa Orthodoksi. Sisi tunaamini kuwa jukwaa nzuri la kutatua mizozo leo kama ilivyokuwa zamani ni kupitia kwa baraza lenyewe. Kuahirisha kikao tena, ni ishara ya kushindwa kufikia kanuni ya uptanisho wa kanisa  hili katika kiwango cha kimataifa.

Hakuna anayetarajia kuwa kikao hiki cha siku kumi kinaweza toa suluhu kwa maswala muhimu na kuleta wiano kwa mambo yaliyomo katika uongozi wa kanisa. Lakini matumaini yetu ni kuwa kikao hiki kitakuwa ni mwanzo wa mapatano na kitafungua ukurasa mpya katika kupatanisha kanisa la Orthodksi kote ulimwenguni. Kikundi cha wachache wenye nia ya kukwaza juhudi za baraza hili hakipaswi kuua ari ya viongozi walio wengi wa Orthodoksi wanaotaka kuwepo na baraza katika sherehe ya Pentekosti.

 Katika karne ya mwisho, Kanisa la Orthodoksi limekuwa ushahidi na kielezo bora katika mafudisho mazito ya dini  na vilevile kuwepo na kizazi kipya cha wafia dini. Baraza Takatifu na Kuu, basi linatupa nafasi ya kuwa na mwanzo mpya kama waorthodoksi. Na wakati huu macho yote ya ulimwengu yanapoelekezwa kwa kanisa la Orthodoksi, tunawasihi viongozi wetu wa dini wasikie mwito wa roho mtakatifu wa kuwa na maridhiano kwa Kanisa letu.